Wanawake
wanaofanya biashara ya kuuza miili na wanaume wanaofanya mapenzi ya
jinsia moja sasa wanatumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi
aina ya Truvada kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo badala ya
kutumia mipira ya kondomu.Picha na Maktaba
Dar es
Salaam. Wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili na wanaume
wanaofanya mapenzi ya jinsia moja sasa wanatumia dawa za kufubaza makali
ya Virusi vya Ukimwi aina ya Truvada kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya
ugonjwa huo badala ya kutumia mipira ya kondomu.(Martha Magessa)
Mwananchi
lilizungumza na baadhi ya wafanyabiashara ya ngono jijini katika maeneo
ya Mwananyamala Hospitali, Komakoma na Vingunguti ambao walisema kuwa
wanatumia dawa hizo kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya VVU ili
kuwaridhisha wateja wasiopendelea mipira hiyo.
Baadhi ya
wafanyabiashara hao walidai kuwa wanatumia Truvada kuzuia maambukizi
pindi wanapokutana na wanaume wakware ambao huwabaka au kuwalazimisha
kufanya mapenzi bila kinga.
"Hizi
dawa tunazipata katika hospitali na wakati mwingine katika maduka
makubwa ya dawa. Kwa sababu zinazuia maambukizi ya Ukimwi na sisi ni
watu ambao tunafanya kazi katika mazingira hatarishi," anasema Leyla
Musa, mmoja wa wanawake hao.
Si hivyo
tu, kwa kuwa hii ni biashara baadhi yao hukubali kufanya mapenzi bila
mipira ili kupata fedha nyingi kutoka kwa wanaume.
Wengine hukimbilia huduma ya PEP
Baadhi ya
wanawake hao wanasema kuwa baada ya kufanya mapenzi na wanaume kadhaa
asubuhi huenda katika kliniki zinazotoa huduma za ARV na kudanganya kuwa
wamebakwa na kisha hupewa huduma za dharura za ARV zinazoitwa kwa
kitaalamu Post-exposure prophylaxis.
Kwa kawaida mtu aliyebakwa au kujikata hupewa dawa aina ya Lamivudine, Zerophidine au Truvada kulingana na uzito wa tatizo.
"Tunatumia
hizi dawa mara kwa mara lakini tunafanya hivyo katika kliniki tofauti
ili tusigundulike," alisema mmoja wao, mkazi wa Mwananyamala, Mariam
Leshaniki.
Kwa
maelezo ya Dk Rachel Baggaley, mtaalamu wa masuala ya Ukimwi wa Shirika
la Afya Duniani anasema dawa za PEP zipo maeneo mengi duniani kwa sasa
na zinafanya kazi kwa ufanisi pia hazina madhara kwa mwanamke.
"Dawa
hizi siyo sumu mwilini, zinaingia kwenye mfumo wako wa damu kabla virusi
havijajizatiti na inavizuia ili mradi uzitumie ndani ya saa 72,"
anasema Dk Baggaley.
Dawa ya
Truvada, ambayo ina mchanganyiko wa dawa aina ya Tenovofir na
Emtricitabine, imethibitishwa kuwa salama kwa kupunguza makali ya VVU
pia kuzuia maambukizi mapya. Dawa hizi zinazotengenezwa nchini India,
zimekuwa msaada mkubwa wa tiba kwenye nchi zinazoendelea.
Post a Comment